Wanamitindo watatu, Anastazia Gura (21) na mapacha, Victoria Casmir
(20) na Victor Casmir wameshinda usaili uliondeshwa na kampuni ya Millen
Magese Group Company Limited chini ya mpango wake wa kuitangaza
Tanzania kupitia fani ya mitindo ujulikanao kwa jina la Tanzania
International Fashion Exposé (TIFEX).
Wanamitindo hao wamefanikiwa kupita katika usaili huo ambao
uliwajumuisha wanamitindo 350 kutoka katika maeneo mbali mbali ya jiji
la Dar es Salaam na mikoa ya jirani.
Kutokana na ushindi huo, wanamitindo hao wanatarajia kuondoka mwishoni
mwa mwezi huu kuelekea nchini Afrika Kusini kushiriki kwa mara ya kwanza
katika historia katika fani ya mitindo ya wiki ya mitindo ya Afrika
Kusini maarufu kwa jina la South Africa Fashion Week.
Akizungumza baada ya usaili huo, Millen alisema kuwa amestushwa sana
na ujio wa wanamitindo mbali mbali mbali waliofika katika usaili huo
japo alitangaza kwa muda mfupi.
Millen alisema kuwa awali alipanga kuchukua wanamitindo wawili,
lakini kutokana na idadi kubwa iliyojitokeza, ameongeza nafasi moja kama
shukrani yake ya witikio huo mkubwa.
Alisema kuwa walipata kazi kubwa sana kuchagua wanamitindo hao
watatu, lakini kwa kushirikiana na wanamitindo maarufu Aminat Ayinde
kutoka kampuni ya America Next top model cycle 12 na Ritha Poulsen,
waliweza kufanikisha zoezi hilo mapema zaidi.
Millen alisema kuwa washindi hao wamepata fursa pekee ya kujitangaza wenyewe kimataifa na kufuata nyayo zake.
Alisema kuwa lengo kubwa la kampuni yake ni kuendeleza fani ya
uanamitindo na vile vile kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake kwa
kupitia fani ya mitindo na hata kwa njia ya utalii.
Aliongeza kuwa japo Tanzania ina wanamitindo wengi na wabunifu, bado
kuna pengo kubwa ukilinganisha na maendeleo ya fani hiyo katika nchi ya
Afrika Kusini na Nigeria.
Alisema kuwa nchi hizo zimepiga hatua kubwa sana na yeye kuhamasika
kuanzisha kampuni yake iliyozinduliwa mwezi Machi mwaka jana kwa lengo
la kuziba pengo hilo na kuleta maendeleo ili wahusika wafaidike na
matunda ya fani yao
Source :http://www.bongo5.com
No comments:
Post a Comment