Tamasha La Matumaini Laacha Historia Dar




JULAI 7, 2012 Jiji la Dar lilisimama kwa takribani saa 16 kupisha tamasha la kihistoria la Usiku wa Matumaini lililotimua vumbi ndani ya Uwanja wa Taifa, Ijumaa Wikienda linakupa ripoti kamili.
Zilikuwa ni saa 16 za hekaheka, vifijo, nderemo, shangwe na burudani ya hali ya juu kuanzia saa mbili za asubuhi mpaka saa sita za usiku, Jumamosi iliyopita ambapo macho na masikio ya wengi viliekezwa uwanjani hapo.

SHUGHULI ILIVYOANZA
Mpango mzima ulianza majira ya saa mbili asubuhi ambapo wasanii chipukizi walifungua pazia la burudani kwa kuwarusha mashabiki waliokuwa wanaendelea kufurika uwanjani hapo.
Wakati hayo yakiendelea, walinzi na wakata tiketi walikuwa na wakati mgumu kuuhudumia umati wa watu uliokuwa umejazana nje ya lango la kuingilia uwanjani hapo huku Bendi ya FM Academia wakiwa wa kwanza kulianzisha kwa kutoa burudanai ya nguvu.

UPAKO WATAWALA
Baada ya wasanii chipukizi kumaliza kutoa burudani, ilifika zamu ya wasanii wa nyimbo za injili ambapo wakali wa muziki huo wakiongozwa na Upendo Nkone, Bahati Bukuku, Bonny Mwaitege, Martha Mwaipaja na Glorious Celebration waliitangaza vyema injili takatifu kwa kupitia karama ya uimbaji. Wakafuatia wasanii chipukizi wanaochana mistari.

BONGO MOVIES VS BONGO FLEVA
Mvua ya burudani iliendelea kunyesha ndani ya uwanja huo ambapo baada ya pilikapilika za mchana kutwa, hatimaye uliwadia wasaa uliokuwa unasubiriwa na wengi.
Wasanii wa kambi mbili hasimu, Bongo Movie inayoundwa na wasanii wa filamu na maigizo ya Kibongo na Bongo Fleva inayoundwa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya, walijitupa dimbani katika mchezo uliovuta hisia za wengi.
Wasanii Jacob Steven ‘JB’, Vincent Kigosi ‘Ray’, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ na wengine wengi walikuwa kivutio kikubwa kwa upande wa Bongo Movie huku wasanii Hamis Baba ‘Baba’, Haroun Kahena ‘Inspekta’, Karama Masoud na wengine kibao wakisakata kabumbu la hali ya juu.
Mpaka kipyenga cha mwisho kinapulizwa, Timu ya Bongo Movie iliibuka kidedea kwa kuinyuka Bongo Fleva goli 1-0, lililofungwa na msanii anayejulikana kwa jina moja la Kiduku. Benchi la ufundi la Bongo Movie, likiongozwa na Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’ lililipuka kwa shangwe wakati kipyenga cha mwisho kikipulizwa.

POLISI WA KIKOSI CHA MBWA WAWAKOSHA MASHABIKI
Baada ya mechi kati ya wasanii wa filamu na wale wa muziki kumalizika, polisi wa kikosi cha mbwa na farasi waliingia uwanjani na kuonesha namna mbwa walivyofuzu katika kukabiliana na uhalifu.
Wakaonesha wanavyoweza kukamata madawa ya kulevya na mabomu. Uwanja mzima ukalipuka kutokana na mashabiki kukoshwa na umahiri wa mbwa hao wanaotunzwa na jeshi la polisi nchini.

WAHESHIMIWA WABUNGE WATOANA JASHO
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaozishabikia timu za Simba na Yanga, nao walijitupa dimbani kucheza mchezo ambao ulikuwa maalum kuhamasisha uchangiaji wa fedha za kujengea mabweni katika shule za sekondari zilizopo vijijini, chini ya Mamlaka ya Elimu Tanzania.
Wabunge Idd Azzan, Zitto Kabwe, Joshua Nasari na wengine wengi waliiongoza timu ya Wabunge wa Simba kukanyaga kandanda safi, huku Mwingulu Nchemba na wenzake wakipiga soka safi upande wa Wabunge wa Yanga.
Mpaka mwamuzi Othman Kazi anapuliza kipyenga cha mwisho, matokeo yalikuwa ni suluhu (0-0).
Mikwaju ya penalti ilipopigwa, Timu wa Wabunge wa Simba iliibuka kidedea kwa kufunga matuta 3-2, shukrani kwa mikwaju ya waheshimiwa Yona Kimube, Amos Makalla na Kikula Abel. Waliokwamisha mpira wavuni kwa upande wa timu ya Yanga ni waheshimiwa Michael Kadege na Sadigo Juma.

NENO LA SHIGONGO, NAPE, ZITTO
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, waandaaji wa tamasha hilo, Eric Shigongo alipanda jukwaani na kutoa nasaha zake kwa dakika kadhaa, aliwasihi Watanzania kurejesha mapenzi kwa nchi yao na kufufua matumaini mapya ya mafanikio.
Naye Katibu wa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliwashukuru wote waliohudhuria tamasha hilo na kueleza kuwa wameshiriki katika mkakati wa kuchangia ujenzi wa mabweni. Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe naye aliwashukuru wote kwa kushiriki kwenye kampeni ya kuzisaidia shule za vijijini kupata mabweni, burudani ikaendelea.

ZAMU YA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA
Baada ya mapambano hayo ya soka, burudani iliendelea ambapo Juma Kassim Kiroboto ‘Nature’ aliwaamsha mashabiki vitini, akafuatiwa na kundi la muziki la Pah One linalofanya muziki pande za Bondeni (Afrika Kusini). Burudani ikaendelea kwa wasanii wengine kama Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ kupanda na kupafomu kwa kiwango cha juu.

WEMA VS WOLPER, NGOMA DROO
Warembo waliolikamata soko la filamu za Kibongo, Jacqueline Wolper na Wema Sepetu nao walitia fora kwa pambano lao kali la masumbwi. Pambano hilo la raundi tatu ambalo lilitarajiwa kumaliza bifu la siku nyingi kati ya wanyange hao, lilitanguliwa na pambano kati ya Kanda Kabongo na Ramadhan Kido, lililomalizika kwa Kabongo kushinda kwa pointi. Mpaka pambano la Wema na Wolper linamalizika kwa droo, uwanja mzima ulikuwa ukishangilia kwa nguvu.
Katika tukio lingine lililowashangaza wengi, baada ya Wema kumaliza pambano, shabiki mmoja ambaye hakufahamika alikotokea, alimvamia msanii huyo akiwa anateremka ulingoni na kumkumbatia kwa nguvu lakini kabla hajamdhuru msanii huyo, polisi walimdaka juujuu na kumshushia kichapo cha haja kabla ya kutolewa nje mzobemzobe.

CHAMELEONE AACHA GUMZO NA VALUVALU
Baada ya mapambano ya ndondi, msanii mkali kutoka nchini Uganda, Joseph Mayanja ‘Chameleone’ aliingia kwa staili yake uwanjani hapo ambapo umati wote ulilipuka kwa shangwe za nguvu wakati msanii huyo akikamua wimbo wake unaobamba kwa sasa, Valuvalu na nyingine nyingi. Mpaka msanii huyo anamaliza shoo, kila mtu alikuwa amesuuzika moyo vilivyo kutokana na burudani ya nguvu aliyoiangusha.

DIAMOND KAMA KAWAIDA YAKE
Yote tisa, kumi ni shoo ya msanii anayeshikilia tuzo tatu za Kili, Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambaye baada ya Chameleone kumaliza shoo, aliingia kwa mbwembwe za hali ya juu.
Wacheza shoo wake waliingia na njiwa weupe ambao waliwaachia uwanjani hapo kabla ya kuanza makamuzi. Diamond aliendeleza makamuzi ya nguvu na kuwadatisha vilivyo maelfu ya mashabiki waliofurika ukumbini humo.
Mpaka inatimu saa sita za usiku, kila aliyehudhuria uwanjani hapo alikuwa ametosheka kwa kiwango kikubwa na burudani ya nguvu iliyoangushwa uwanjani hapo kuanzia saa mbili za asubuhi.

No comments:

Post a Comment